Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA-, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, alieleza katika utangulizi wa mkutano wake na waandishi wa habari kila wiki leo Jumatatu kuwa: Mzairu wa kwanza kabisa aliyetumwa na Iran kushiriki katika maombolezo ya Arbaeen mwaka huu huko Karbala Tukufu, alikuwa Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ambaye katika mwenendo wake hakuwa na mfano wa kuigwa isipokuwa Imam Hussein (Amani iwe juu yake).
Akiashiria uhalifu uliofanywa na Marekani pale ilipotekeleza shambulio dhidi ya familia ya Kiirani katika kisiwa cha Qeshm kusini mwa nchi hiyo, kwa kutumia mabomu yenye uzito wa karibu kilo elfu moja, jambo lililopelekea kuuawa shahidi kwa baba, mama na mtoto wao wa miaka miwili, na kujeruhiwa kwa watoto wengine wawili matineja wa familia hiyo.
Alisema: Uhalifu wa Marekani kwa mara nyingine tena katika wiki iliyopita umegusa ardhi ya Iraq; ambapo wakati wa shambulio la anga lililotekelezwa na Marekani na washirika wake dhidi ya Iraq, raia kadhaa wapendwa wa Iran waliuawa shahidi, nao ni: Amir Abbas Derhamforoush, Ali Asghar Astan, Morteza Akbari, Abolfazl Mottaghi, na Mahmoud Rostami.
Pia aliashiria kuuawa shahidi kwa kijana wa Kiirani kutoka mji wa Bandar Anzali kaskazini mwa nchi, kufuatia shambulio lililotekelezwa na utawala wa Ukraine dhidi ya meli ya kibiashara ya Iran katika Bahari ya Kaspi.
Makubaliano na Sultanate ya Oman ni Sharti la Lazima Kufungua Mlango-Bahari wa Hormuz, lakini Halitoshi / Hatufanyi Mazungumzo Yoyote na Marekani kwa Sasa
Kuhusu mazungumzo kati ya Iran na Sultanate ya Oman, alisema: Mazungumzo yetu yanafanyika na Sultanate ya Oman, na tunazingatia kufikia makubaliano kuhusu mfumo unaohakikisha usafiri salama wa baharini kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz. Tunatafuta kuamua njia mapema iwezekanavyo kwa kushauriana na kushirikiana na Sultanate ya Oman, njia ambayo itakuwa ya muda, ambapo tutaweza kuulinda usafiri wa baharini katika Mlango-Bahari wa Hormuz.
Aliongeza: Kwa hiyo, mazungumzo haya ni ya nchi mbili kati ya mataifa mawili ya pwani. Wengine wanaweza kuchukua nafasi ya kujenga au ya uharibifu ndani yake, lakini suala hili linahusu Iran na Oman pekee. Ama kuhusu nini kitatokea katika hatua inayofuata, uamuzi unapaswa kuchukuliwa kuhusu hilo.
Nilitangaza pia jana usiku kwamba makubaliano juu ya njia salama ya harakati za meli kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz ni sharti la lazima ili kufungua tena mlango huo, lakini sio sharti linalotosha. Mlango-Bahari wa Hormuz haukufungwa kwa sababu ya tofauti za maoni kati ya Iran na Oman, bali mlango huo umekuwa ukikabiliwa na matatizo tangu mwezi Machi 2026 kutokana na uvamizi wa kijeshi wa Marekani na utawala wa Kizayuni.
Baghaei aliongeza: Mradi tu vitendo viovu vya Marekani vinaendelea, mradi tu mzingiro wa baharini uliowekwa dhidi ya Iran upo, na mradi tu uvamizi wa kijeshi wa Marekani dhidi ya Iran na maslahi yake unaendelea, na ilhali ukiukwaji wote uliofanywa na Marekani katika kipindi hiki chote ukiendelea, ni jambo la kawaida kwamba hakutakuwa na mabadiliko yoyote yanayoonekana katika hali ya Mlango-Bahari wa Hormuz.
Kwa hiyo, msisitizo wa mazungumzo na Sultanate ya Oman utakuwa kwenye mada hii, wakati masuala yanayohusu Iran na Marekani yanapaswa kujadiliwa katika hatua za baadaye ili kuona wapi hali itakapoishia.
Baghaei alisisitiza kuwa "kile kinachotujali sisi ni maslahi ya kitaifa, na kwamba sisi katika vyombo vya diplomasia, tunahesabiwa kuwa waaminifu wa maslahi ya kitaifa na usalama wa taifa la Iran."
Tunathamini Juhudi za Nchi za Ukanda Huu Kuzuia Kuzuka kwa Vita... na Kilichomzuia Adui Kukuza Vitendo Vyake Viovu Dhidi ya Iran ni Nguvu ya Nchi na Uwezo Wake wa Kuzuia
Akijibu swali kuhusu «madai yaliyoenezwa na vyombo vya habari vya Magharibi kwamba suala la shambulio lililodaiwa dhidi ya Iran lilifutwa wakati wa mawasiliano kati ya Mohammed bin Salman na Donald Trump. Je, unadhani Saudi Arabia ilijaribu kusimamisha uvamizi huu, au ni jibu madhubuti la Iran ndilo lililozuia utekelezaji wake?», Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje alisema: Hisia ya nchi zote za ukanda huu ya kuwajibika kuelekea mustakabali wa eneo hili na kila kitu kinachoweza kukabiliana nacho ni jambo la baraka. Vita vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran si vita dhidi ya nchi moja tu, bali ni vita dhidi ya ukanda mzima na dhidi ya usalama wa nchi zake zote.
Baghaei aliongeza: Tumeshuhudia katika miezi hii mitano kwamba uwepo wa kijeshi wa Marekani katika ukanda huu na matumizi ya ardhi na uwezo wa nchi za Ghuba ya Uajemi, umepelekea kuongezeka kwa ukosefu wa usalama na kutokuwepo kwa utulivu kwa nchi zote za ukanda huo. Kwa hiyo, ni jambo la kawaida kwamba nchi za ukanda huu zijaribu kuzuia kuzorota kwa hali hii. Tunathamini juhudi hizi, lakini uzoefu umetuthibitishea kwamba kile kinachoweza kumzuia adui hatimaye kukuza vitendo vyake viovu dhidi ya Iran, ni nguvu ya nchi na uwezo wake wa kuzuia.
Pakistan Ndio Msuluhishi Kati ya Iran na Marekani
Akijibu swali kuhusu «ripoti zilizochapishwa hivi karibuni kuhusu usuluhishi wa China katika uhusiano wa Iran na Marekani kuhusu Mlango-Bahari wa Hormuz. Je, usuluhishi huu umethibitishwa ili kupunguza mivutano katika ukanda huo na je, uko katika hatua ya utekelezaji?»,
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje alisema: Msuluhishi katika masuala yanayohusu Iran na Marekani ni Pakistan, na Qatar inatoa usaidizi katika matukio yanayohitaji hivyo. Tuna uhusiano wa kirafiki sana na China na tunadumisha ushirikiano wa karibu katika nyanja zote zenye maslahi ya pande zote mbili.
Baghaei aliongeza: China, kama sisi, ina wasiwasi kuhusu hatua ya Marekani ya kuongeza mbinu yake ya upande mmoja, yenye uharibifu na uadui. Pia ina wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa mgogoro na ukosefu wa usalama katika ukanda huo. Kwa hiyo, marafiki zetu wa China wanajaribu na kuweka juhudi zao nzuri kuzuia kuzorota kwa hali hiyo. China inasaidia kama zilivyo nchi nyingine kadhaa; lakini haiwezi kusemwa, kwa maana halisi ya neno, kwamba tumeongeza msuluhishi mpya kwenye orodha ya wasuluhishi waliopo.
Suala la Yemen Linahusu Wayemeni Wenyewe, na Suluhu Yake ni Mazungumzo / Tuhuma Dhidi ya Iran za Kupanua Vita ni Upotoshaji wa Ukweli
Akijibu swali kuhusu «kama kuna tuhuma zilizoelekezwa dhidi ya Iran katika siku za hivi karibuni, sambamba na mashambulizi ya kujitegemea ya Ansarullah ya Yemen na madai yasiyothibitishwa kuhusu shambulio la ndege isiyo na rubani ya Muungano wa Muqawama wa Iraq kwenye vifaa vya mafuta vya Saudi Arabia, kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatafuta kufungua mipaka mipya na kupanua wigo wa vita kijiografia.
Ni nini jibu lenu kwa tuhuma hizi na madai haya?», Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje alisema: Nina hakika kwamba anayevumisha madai haya anakusudia kupotosha ukweli. Miezi mitano iliyopita sio kipindi kirefu kiasi cha mtu kusahau. Kabla ya miezi mitano, mwezi Machi, tulikabiliwa na uhalifu na uvamizi wa kijeshi kutoka kwa Marekani na utawala wa Kizayuni. Je, Iran ilifungua mpaka? Tangu siku ya kwanza ya vita vilivyowekwa na Marekani na utawala wa Kizayuni, ardhi na uwezo wa nchi za ukanda huu vilitumiwa kutekeleza kitendo na uvamizi dhidi ya Iran. Je, sisi ndio tuliopanua mipaka?
Baghaei aliongeza: Suala ya Yemen linahusu Wayemeni wenyewe. Tumetangaza msimamo wetu kuhusu Yemen. Nchi hii inateseka tangu muda mrefu kutokana na mzingiro wa kidhalimu, na tumesema mara kwa mara kwamba suluhu ya mgogoro wa Yemen lazima ifanyike kupitia mazungumzo na kwa msingi wa ramani ya njia iliyofikiwa makubaliano tangu muda fulani kati ya pande zinazohusika. Kwa hiyo, kuhusisha suala lolote na vita vilivyowekwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kisingizio tu cha kukimbia uwajibikaji na ni ishara ya unyonge.
Wao wenyewe ndio walioanzisha mgogoro huu. Moto waliouweka, kwa asili yake, utasambaa. Haiwezekani kuwasha moto dhidi ya nchi fulani kisha tukatarajia kwamba moto huo utajifungia kwenye eneo lililolengwa pekee. Uwajibikaji wa kila kinachotokea leo katika ukanda huu, na hata nje yake, unamwangukia kikamilifu Marekani; kama mwanzilishi wa uvamizi huu wa kijeshi, na kila aliyetaka, kwa bahati mbaya, na kwa namna tofauti, kufanya kazi kama washirika wa wavamizi.
Maoni yako